Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametaka kusitishwa mara moja kwa vita nchini Yemen ambako muungano wa nchi za ghuba zikiongozwa na Saudi Arabia zimekuwa zikifanya mashambulizi ya angani dhidi ya raia madhulumu wa Yemen na wanapinduzi wa kishia kutoka jamii ya Houthi.
Ban Ki Moon amesema taifa la Yemen lilikuwa tayari katika mzozo hata kabla ya mapigano hayo kupamba moto na kuongeza vita hivyo vimesababisha hali ya kibinadamu nchini humo kuwa hata mbaya zaidi. Ban Ki Moon amezitaka pande zote zinazozana katika taifa hilo masikini la Mashariki ya kati kusitisha vita hivyo mara moja na kuongeza kuwa Saudi Arabia imemhakikishia kuwa inafahamu kuwa sharti mzozo wa Yemen utafutiwe ufumbuzi wa kisiasa. Hayo yanakuja huku mjumbe mpya wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen akitarajiwa kuteuliwa hii leo baada ya Jamal Benomar kujiuzulu.